image in blog

image in blog
mindu

Wednesday, November 20, 2013

Mmwalimu Nyerere na Taifa TANZANIA katika RUSHWA na MUUNGANO

Mwalimu Nyerere aliona mbali
mwalimu nyerere
14 OKTOBA 1999, Tanzania, Afrika na dunia nzima ilipatwa mshituko baada ya kutangaziwa kuwa mwanamapinduzi na mpigania haki na usawa duniani, baba wa taifa la Tanzania, mwanaAfrika mzalendo wa kweli, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ameaga dunia huko katika hospitali ya Mt. Thomas, Uingereza alikokuwa akitibiwa.
Leo ni miaka 13 sasa.  Taifa na wapenda haki na uadilifu wote duniani tunamkumbuka.  Alikuwa mwalimu wa kweli.  Mwana wa kweli wa Tanzannia na Afrika.
Tunapomkumbuka, ningependa tujikumbushe mambo mawili aliyoyazungumza panapo Machi 13, 1995 alipokuwa akizungumza na Klabu ya Waandishi wa Habari Tanzania.  Mwalimu, pamoja na mambo mengine mengi ya msingi, alizungumzia rushwa na muungano.
Kuhusu rushwa, katika mengi aliyoyazungumza, pia alisema;
‎"Serikali ya wala rushwa haikusanyi kodi. Itabaki kufukuzana fukuzana na vijitu vidogo vidogo mabarabarani hivi tu basi. Hili jambo ni sheria kama ile ya kwanza niliyowaambiwni kuhusu ubaguzi, mkianza ubaguzi, mtaendelea moja kwa moja; hamna mahali pa kusema simama hapa. Mkisha kuwa wala rushwa, mtaabudu wenye mali. Mimi ni Mkristu, sijui Kuruani inasema nini, lakini msahafu wa Kikristo, Injili, ambayo na Waislamu wanamkubali Nabii Issa, kwa maneno yake mwenyewe "huwezi kutumikia mabwana wawili, mmoja fedha, mwingine Mungu; haiwezekani, utachagua katika wawili hao".
Akazungumza pia kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao umekumbwa na misukosuko kadhaa wa kadha kutoka kwa watu wasioitakia mema nchi yetu.  Mwalimu Nyerere akazungumza mambo mengi sana, kati ya hayo, akasema;
‎"Watu wazima wamezungumza Muungano, kwamba tuuvunje au tuendelee. Ilikuwa ipo hatari ya kuvunjika na wala haijaisha. Watu wamezungumza Uzanzibari, na baadhi ni viongozi wetu, wanajivunia Uzanzibari. Nadhani wengine wanafikiria hata kujitenga. Wapo si wengi; lakini wapo. Kujitenga maana yake ni kuvunja nchi ivunjike tusiwe na nchi moja, tuwe na nchi mbili. Ni jambo linalozungumzwa. Tunataka kiongozi na viongozi watakaoelewa hivyo. Huku kuzungumza Uzanzibari si fahari. Si jambo la fahari. Hatima yake tutavunja nchi. Zanzibar, mtu mwenye akili hawezi kufikiri Uzanzibari ni fahari: hana akili.

Hawezi akautukuza Uzanzibari kwa kujiita 'sisi Wazanzibari' na 'wao Watanganyika'.

Nadhani ile ina usalama ndani yake. Kwamba Uzanzibari ule, Utanganyika ule una usalama ndani yake. Hatima yake Zanzibar itajitenga. Zanzibar ikijitenga kutokana na ulevi tu; sisi Wazanzibari na wao Watanganyika wakumbuke kwamba Muungano ndio unaowafanya wanasema 'sisi Wazanzibari' 'wao Watanganyika'. Nje ya Muungano, hawawezi kusema hivyo: kuna 'wao Wapemba' na 'sisi Waunguja'.

Nataka mjue hivyo. Nje ya Muungano hakuna 'sisi Wazanzibari' 'wao Watanganyika'. Hakuna. Kinachowafanya mjiite 'sisi' ni ubaguzi wa kuwabagua Watanganyika. Wakiisha kuwabagua Watanzania Watanganyika, ile dhambi ya ubaguzi, haifi inaendelea. Dhambi ya ubaguzi ukisha kuitenda inaendelea: ni kama ukila nyama ya mtu utaendelea kuila. Mtamaliza mtatengana na Watanganyika halafu, mara mtakuta kumbe 'sisi' 'si Wazanzibari'. Kuna 'Wapemba' na 'Waunguja'. Wapemba watapata msukosuko kidogo aaolololo!

Mtakuta kumbe kuna Wazanzibari na Wazanzibara! Hamtakaa salama. Hamwezi mkakaa salama baada ya kutenda dhambi ya kuwabagua watu wa nchi yenu ile ile moja mkawaita 'wale wao' na 'hao sii'. Dhambi ile haiishii hapo. Ndivyo historia ilivyo; ni sheria ya historia siyo sheria ya Mwalimu Nyerere. Huwezi kufanya ubaguzi wa namna hiyo halafu dhambi ile ikuache hapo hapo. Hapana itakuandama."
Hivyo ndivyo ninavyomkumbuka Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (1922-1999) kwa siku ya leo.
Tafakari!
Mwenyezi Mungu akupumzishe kwa amani.  Amina.
 
ibrahim mindu
by Mindu jr.... The future

No comments: