Hatua hiyo inafuatia kesi kabambe iliyopo ICC ambapo rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta pamwe makamu wake William Ruto wanatuhumiwa kwa kusababisha vurug za uchaguzi wa Kenya mwaka 2007. Kumekuwa na jitihada za makusudi kutoka ndani ya Kenya, hususani kwa wabunge wa Jubilee wakitaka Kenya kujiondoa kwenye Mkataba wa Roma ulioanzisha mahakama hiyo.
Jitihada hizo zimetua rasmi jijini Adis Ababa ambapo chombo kikubwa zaidi barani Afrika kinaketi. Sote tunafahamu kwa nini ni Kenya na Sudan walio mstari wa mbele kushawishi nchi 34 za Kiafrika zilizotia saini Mkataba wa Roma kuisusia ICC. Wakati rais wa Kenya na makamu wake wakiwa na kesi, naye rais wa Sudan, Omar al-Bashir alishatolewa hati ya kukamatwa kwake. Ndiyo sababu iliyoifanya hata Marekani kumnyima viza ya kuingia nchini humo kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa majuma machache yaliyopita.
Balozi wa Sudan huko Adis Ababa, bwana Abdul-Rahman Siralkhatim amenukuliwa jana akidai kuwa kitendo hicho cha viongozi wa Kiafrika kinatarajiwa kuwa cha kihistoria zaidi dhidi ya ukandamizaji unaofanywa na mataifa ya Magharibi kwa nchi za Kiafrika.
Kwa nini nchi za Kiafrika haziitaki ICC? Ni kwa sababu ya ukandamizaji wa Kimagharibi dhidi ya nchi zetu za Kiafrika? Kwa mtazamo wangu, sababu ni zaidi ya hiyo. Kama tatizo ni ukandamizaji wa mataifa ya Kimagharibi, hapana shaka nchi za Kiafrika zingekuwa mstari wa mbele kusimama imara kwa pamoja kupinga ukandamizaji wa kiuchumi unaofanya na wawekezaji wa mataifa ya Ulaya na Asia.
Hizi nchi zinazosema mataifa ya Magharibi yanatukandamiza Waafrika kwa kupitia ICC ndizo zilizo mstari wa kwanza kutoa misamaha mikubwa ya kodi kwa makampuni makubwa ya Magharibi yanayokuja kwa mwamvuli wa uwekezaji huku yakikwangua pasi huruma rasilimali zote za Afrika. Busara kubwa kwa nchi za Afrika, bara lenye wakazi zaidi ya bilioni moja ikiwa ni zaidi ya asilimia 15 ya idadi ya watu ulimwenguni, ingekuwa ni kwa nchi hizi kuikata mirija ya unyonyaji kutoka kwa mataifa tajiri duniani. Hili lingewezekana kwa nchi za Kiafrika kuungana pamoja katika kuzisimamia vema rasilimali zilizopo. Kama nchi ya China imefanikiwa ikijivunia idadi yake ya watu, nchi za Afrika zinashindwa nini?
Leo hii, nchi za Kiafrika zinaiona ICC kama adui yao mkubwa kwa kuwa tu imewagusa wakubwa wenzao. Lakini tujiulize swali la msingi. Si kweli ukatili dhidi ya binadamu ulitokea Kenya ama Sudan? ICC inaweza ikawa na matatizo yake ya kimfumo na utendaji wa kazi. Tunarejea kwenye busara ya kisheria, makosa mawili hayalihalalishi kosa la pili.
Nchi za Kiafrika zinatambua vema juu ya Wakenya zaidi ya 1000 waliopoteza maisha kufuatia vurugu zile. Zinafahamu vema juu ya wengine zaidi ya laki sita waliopoteza makazi yao. Si hilo tu, zinafahamu vema juu ya ripoti ya kurasa 529 ya Tume ya Waki iliyoundwa kuchunguza kiini na wasababishi wa kadhia ile mbaya kabisa katika historia ya taifa hilo la Afrika Mashariki. Bila shaka pia, nchi hizi za Kiafrika zinakumbuka vema namna mwendesha mashtaka wa ICC wa wakati huo Luis Moreno-Ocampo alivyozipa mamlaka za Kenya mwaka mmoja ili ziweze kuunda chombo cha ndani cha kuwahukumu watuhumiwa hao. Kenya ikapuuza kufanya hivyo.
Leo hii, jijini Adis Ababa, viongozi wetu wanatuambia mambo ya Afrika yatasimamiwa na Waafrika wenyewe. Tunajifunza nini kwa mfano huu wa Kenya ilipopewa mwaka mmoja wa kuunda mahakama ya ndani nayo ikapuuza kufanya hivyo? Tunawaza nini kujisahaulisha kuwa hatua ya ICC kuwafungulia kesi Uhuru na wenzake ilitokana nasi Waafrika wenyewe kupuuza agizo la kujihukumu wenyewe?
Endapo nchi za Afrika zitajitoa kwenye Mkataba wa Roma na hivyo kuamua kutoipa ushirikiano ICC, litakuwa pigo kubwa mno kwa Waafrika. Hatua hiyo itafungua milango kwa ukandamizaji dhidi ya haki za kibinadamu. Itafungua milango kwa matukio mengi ya ukatili dhidi ya binadamu huku viongozi wa Afrika wakijivunia kutowajibika pahala popote katika ngazi ya kimataifa.
Wasiwasi wangu ungalipo. Kiongozi anapoukataa mfumo wa kisheria unaomsimamia namna afanyavyo kazi zake, hapana shaka anataka kuwa juu ya sheria. Madhara ya kuwa na viongozi walio juu ya sheria ni makubwa mno kwa watawaliwa ambao kwa kawaida ni watu wa chini wasio na nguvu yoyote nje ya sheria kuuondoa ukandamizaji wowote dhidi yao.
Hatua hii ya viongozi wa Afrika inapaswa kutazamwa kwa jicho la usaliti dhidi ya Waafrika wenzao. Inapaswa kueleweka kama hatua inayokusudia kupiga mhuri wa moto kwenye mamlaka zisizo na kikomo kwa viongozi wa Afrika.
Kama sivyo, kwa nini nchi za Afrika zinaihara ICC?
ibrahim mindu
by mindu jr.... The future
No comments:
Post a Comment