image in blog

image in blog
mindu

Friday, January 31, 2014

UTALII WA NDANI WA TANZANIA NI WA WATANZANIA WENYEWE

Watalii wa ndani wakifurahia utalii wa kutembea kwa miguu katika hifadhi ya taifa ya Arusha jirani kabisa na kundi la nyati. “PAMOJA na kusikia wakitangaza hifadhi za taifa tulizonazo, huu ni muda muafaka kwa wananchi na watu mashuhuri nchini wakiwemo wanahabari kuzitembelea ili kukuza utalii wa ndani,” anasema Ofisa Mahusiano Mwandamizi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Catherine Mbena. Kaimu Mkurugenzi wa Mipango na Utalii wa Tanapa, Dk Ezekiel Dembe anasema lengo ni kufikisha watalii milioni 2.5 ifikapo mwaka 2015. “Tunataka utalii katika hifadhi zetu ukue kwa kuzingatia ubora sio ukubwa ili kulinda ikolojia ya maeneo yaliyohifadhiwa,” Dk Dembe anasema. Hifadhi hizo ni pamoja na Mlima Kilimanjaro, Serengeti, Tarangire, Manyara, Arusha, Mkomazi, Mikumi, Ruaha, Katavi, Kitulo, Udzungwa na vivutio vingine vingi. Mbali na uoto wa asili uliopo katika hifadhi hizo, kuna aina mbalimbali za wanyama kama Simba, Tembo, Twiga, Nyati, Chui na makundi makubwa ya pundamilia, twiga na nyumbu. Kimsingi, umashuhuri wa watu hupimwa kutokana na yale wanayofanya katika jamii, idadi ya watu wanaowaunga mkono, na wengine wanaotaka kuwasikia, kuwasoma, kuwatazama au kufanya mazuri wanayofanya, Mbena anasema. Kitendo hicho huwafanya watengeneze masoko kwa sababu ya kukubalika kwao na kuifanya jamii ichague au ipende kufanya mazuri wanayoyafanya. Mbena anawataja baadhi ya watu mashuhuri wanaoweza kusaidia kukuza utalii wa ndani kwa kutembelea vivutio tulivyonavyo kuwa ni pamoja na viongozi wa Serikali, dini, taasisi za umma na zisizo za kiserikali; wana siasa, michezo, muziki, waigizaji, wanahabari na wengine wengi. Anasema watu mashuhuri wana maslahi fulani kwa umma na huongoza kwa muonekano kwenye vyombo vya habari ambavyo ni daraja la mawasiliano kati yao na wananchi wengine. Utafiti uliofanywa nchini Australia na taasisi ya Future Foundation mwaka 2007 unaonesha kwamba asilimia 55 ya wanawake na asilimia 39 ya wanaume wanapenda kusikia na baadhi yao kuiga mazuri yanayofanywa na watu mashuhuri. “Kwa mfano wapo Watanzania wamepanda mlima Kilimanjaro baada ya kusikia msanii maarufu wa Bongo Fleva, Lady Jay D kapanda mlima huo,” Mbena anasema akidhihirisha jinsi watu mashuhuri wanavyoweza kusaidia kukuza utalii wa ndani kama watatembelea hifadhi mbalimbali nchini. Anasema Watanzania wengine wametembelea hifadhi zetu baada ya kusikia na kuona kwenye vyombo vya habari wasanii wa kundi la wachekeshaji la The Original Comedy wakitembelea baadhi ya hifadhi ikiwemo hifadhi ya pili kwa ukubwa barani Afrika ya Ruaha. Mbena anawataja watu wengine mashuhuri ambao wamesaidia kutangaza hifadhi zetu ndani na nje ya nchi baada ya kutembelea hifadhi hizo kwa nyakati tofauti kuwa ni pamoja na Rais Jakaya Kikwete na Mkuu wa Majeshi mstaafu, Jenerali Mrisho Sarakikya. Na kwa upande wa watu mashuhuri kutoka nje ya nchi, Mbena anawataja baadhi yao ambao kwa kiasi kikubwa wamesaidia kutangaza hifadhi zetu kuwa ni pamoja na muigizaji wa sinema za kibabe Arnold Schwarzenegger wa Marekani aliyetembelea hifadhi ya Katavi. Wengine ni aliyekuwa nyota wa klabu ya Manchester United, David Beckham aliyetembelea Hifadhi ya Serengeti. Mwingine ni Muigizaji maarufu kwa jina la Rambo, Silyveter Stallone wa Marekani aliyetembelea Hifadhi ya Udzungwa na zingine za Kaskazini. Naye mmoja wa matajiri wakubwa duniani na mmiliki wa klabu ya Chelsea ya Uingereza, Roman Abromovich alipanda mlima Kilimanjaro katika tukio lililovutia matajiri wengine wengi ambao kwa mujibu wa Ofisa Mahusiano wa Tanapa, Mbena wanatarajia kuja na kufanya utalii katika mlima huo. Mbena anasema kitendo cha Abromovich kupanda mlima huo si tu kwamba kimeamsha ari kwa matajiri wenzake kuja nchini na kujionea vivutio mbalimbali vilivyopo, bali pia kimeamsha hali kwa Watanzania hususani wale ambao ni wapenzi wa klabu ya Chelsea kuupanda mlima huo. Akiwa amevaa jezi inayotumiwa na klabu hiyo, Jackson Mtambalike aliyekutwa na mwandishi wa makala haya nje ya lango la kuingilia katika hifadhi ya mlima huo hivi karibuni alisema “baada ya kusikia Abromovich kapanda mlima huu, niliweka dhamira ya kuwa mmoja wa mashabiki wa Chelsea kupanda mlima huu ili kuunga mkono kilichofanywa na mmiliki wa timu hiyo.” Katika tukio la hivi karibuni, mtoto wa Rais mstaafu wa Marekani Bill Clinton, Chelsea Clinton na Waziri Mkuu wa Thailand, Yingluck Shinawatra kwa nyakati tofauti walitembelea Hifadhi ya Tarangire na Serengeti. Chelsea Clinton alinukuliwa na Jarida la Tanapa Today la mwezi Julai-Septemba, 2013 akiwa Hifadhi ya Tarangire akisema “ Nikiwa hapa Tanzania nimetembelea moja ya hifadhi ambayo asasi ya Wildlife Conservation Society inafanya utafiti wa tembo na kushirikiana na Serikali ya Tanzania kulinda kiumbe hicho.” Chelsea aliyeona tembo mtoto mwenye miezi mitatu akicheza huku mama yake mwenye miaka zaidi ya 30 akionekana kumlinda anasema “hawa ni viumbe wa kuvutia na wasio na hatia, ni muhimu kwetu sote tukawalinda.” Mratibu wa Mradi wa Kuboresha Mtandao wa Maeneo ya Hifadhi Kusini mwa Tanzania (SPANEST), Godwell ole Meinng’ataki anasema Tanzania imekuwa ikipata fedha nyingi kutoka kwa watalii wanaoingia hifadhini kuangalia tembo na wanyama wengine. “Bila shaka kiasi cha fedha wanachopata majangili wa meno ya tembo hakiwezi kuwa sawa na kile kitokanacho na utalii; ni muhimu tembo na wanyama wengine wakaendelea kuwepo kwa faida ya sasa na kizazi kijacho,” anasema. June mwaka huu 2013, Rais wa Sri Lanka Mahinda Rajapaksa naye alitembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti na kuvutiwa na mandhari yake nzuri iliyosheheni wanyama mbalimbali. “Haya ni maajabu ya dunia, sijawahi kuona makundi makubwa ya nyumbu na nyati kama niliyoyaona Serengeti; nitawaambia watu wangu na naahidi kurudi tena na tena nikiwa na familia yangu,” anasema. Muongoza watalii wa mjini Arusha, Jackson Mollel anasema kwa miaka mingi watangazaji wamewatumia watu mashuhuri kutangaza bidhaa zao na kuongeza masoko ya huduma au bidhaa zao. Tunataka watu mashuhuri wa ndani ya nchi watembelee hifadhi zetu, hii itahamasisha Watanzania wengine kutembelea na hatimaye kuinua utalii wa ndani, Mollel anasema. Kaimu Mkurugenzi wa Mipango na Utalii wa Tanapa, Dk Dembe anasema wakiwa katika lengo la kupokea watalii milioni 2.5 ifikapo 2015, idadi ya watalii wa ndani na nje inazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka. Lengo la Tanapa lilikuwa kupokea wageni milioni moja ilipofika mwaka 2010, lakini hadi sasa hifadhi zetu zinapokea watalii wanaokaribia milioni 1.5 huku zaidi ya asilimia 90 wakiwa ni wale wanaotoka nje ya nchi. Anasema lengo la kupokea wageni milioni 2.5 linatakiwa liende sambamba na uboreshaji wa miundombinu ya barabara ndani ya hifadhi, viwanja vya ndege na huduma kwa wageni. “Zipo huduma za waongoza watalii na usafiri, malazi na vyakula ndani na nje ya hifadhi, vyote kwa pamoja ni lazima viendelee kuboreshwa ili viendane na mahitaji tofauti ya watalii,” anasema. Dk Dembe anasema katika kuboresha huduma kwa watalii tunataka “waongoza watalii na madereva wazingatie taratibu za hifadhi; tutawapa mafunzo madereva wote wanaoingia hifadhini.” Anasema madereva hao watapewa vitambulisho na endapo watakiuka taratibu za hifadhi watanyang’anywa vitambulisho vyao na kuzuiwa kubeba watalii hifadhini kwa usalama wa vivutio ndani ya hifadhi na watalii wenyewe. Anasema safari na utalii ni vitu vinavyokwenda pamoja hivyo ni muhimu kwa wadau wakaboresha sekta ya usafiri na kutoza gharama kwa kuzingatia hali halisi ya uchumi hasa kwa Mtanzania wa kawaida. “Kwa upande wetu tunaendelea kuimarisha mtandao wa barabara ndani ya hifadhi na lengo letu ni kuona barabara hizo zinajengwa kwa kiwango ambacho zitapitika kwa mwaka mzima,” anasema. Kwa upande mwingine Serikali ya Rais Kikwete nayo inaendelea kuboresha miundombinu ya barabara nje ya hifadhi ambazo nyingi zinajengwa kwa kiwango cha lami.Kuhusu huduma ya usafiri wa anga, Dk Dembe anasema mbali na hifadhi za Kaskazini kuwa na kiwango cha kuridhisha, kukamilika kwa uwanja wa Songwe Mbeya na baadhi ya kampuni za ndege kuanzisha safari kwa kutumia viwanja vya mikoa kutaboresha huduma hiyo kwa mikoa ya Kusini. Katika kuinua utalii wa ndani, Martin Jones ambaye ni mtalii kutoka Australia aliyetembelea Hifadhi ya Serengeti hivi karibuni anasema “huduma ya usafiri haipaswi kuwa kikwazo kwa Watanzania.” “Kuna kampuni za usafiri wa watalii zinatoza kwa siku Dola za Kimarekani 250 (sawa na zaidi ya Sh 400,000) kwa mtalii mmoja; kiasi hicho ni kikubwa kwa watalii wa nje lakini ni kikwazo kwa watalii wa ndani,” anasema. Naye Lizy Stewart mtalii kutoka Uingereza aliyetembelea Hifadhi ya Tarangire hivi karibuni anasema sekta ya usafiri inatakiwa iwe sekta ya huduma ikiwa ni ‘sehemu ya uchumi wa taifa inayohudumia msafiri anayetembelea eneo nje ya eneo analokaa au kufanya kazi.’ Mkurugenzi wa Kampuni ya Tatanca Tours ya mjini Iringa, Denis Ngede anasema “kuongezeka kwa watalii wa ndani kutasaidia kupunguza gharama za uendeshaji ambazo kwa asilimia kubwa hutegemea watalii kutoka nje na hivyo kupungua kwa gharama za safari.” Mmoja wa watalii wa ndani aliyetembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Tarangire, Arusha, Manyara na Mlima Kilimanjaro, Tukuswiga Mwaisumbe anasema “nimeandika historia katika maisha yangu.” Mwaisumbe (40) anasema katika historia ya maisha yake hakuwahi kufikiria kutembelea hifadhi hizo akihofia gharama kubwa. “Kwa Mtanzania wa kawaida ni ngumu kutembelea hifadhi hata kwa siku moja akiwa peke yake; kitakachomuongezea gharama ni usafiri wa kukodi, lakini wakiwa katika makundi ni rahisi kutembelea hifadhi kwani gharama itakuwa ya kuchangia,” anasema. Akitoa mfano, Ofisa Utalii wa Tanapa wa Ofisi ya Utalii ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Risala Kabongo anasema gharama ya kukodi Coaster yenye uwezo wa kupakia watu 25 kutoka Iringa Mjini hadi Hifadhi ya Ruaha ni Sh 500,000. “Kiasi hicho kinamfanya kila mtu achanngie Sh 20,000 ambayo kimsingi ni nafuu sana ikilinganishwa na Sh 500,000 anazoweza kulipa mtu mmoja kwa kukodi Toyota Land Cruiser kwa siku moja,” anasema. Akizungumzia gharama za kuingia hifadhini, Kabongo anasema ni kati ya Sh 1,000 na Sh 15,000 kwa mtu; gharama hiyo ikizingatia makundi ya wanafunzi, watoto na watu wazima. Kuhusu huduma za malazi na vyakula, Dk Dembe anasema Kanda ya Kaskazini inazidi kupiga hatua kubwa na kwamba mkakati wao ni kuwashirikisha wadau kuboresha sekta hiyo katika Kanda ya Kusini. “Tunahamasisha wafanyabiashara waanzishe kampuni za utalii katika mikoa ya Kusini; lakini pia tutafanya makongamano ya uwekezaji Februari mwakani,” anasema. Kwa kupitia makongamano hayo, Tanapa itatangaza kuuza maeneo ya uwekezaji wa hoteli za kitalii katika hifadhi zake na watakaopata maeneo hayo watatakiwa kuanza kuwekeza katika kipindi cha miezi sita. Katika mchakato wa kuifanya sekta ya utalii iendane na wakati, Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki hivi karibuni alinukuliwa akiahidi kwamba Serikali itazifanyia marekebisho sheria, sera na kanuni zinazohusu sekta ya utalii ili ziendane na wakati. Alikuwa akijibu hoja mbalimbali zilizotolewa na wabunge pamoja na wawakilishi wa Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (Tato) kwenye semina ya kujadili changamoto na faida ya sekta ya utalii. Kagasheki anasema sheria, sera na kanuni zinazoongoza sekta ya utalii zilizopo zimepitwa na wakati na zimekuwa zikichangia kudorora kwa sekta hiyo ikiwemo kuwavutia wawekezaji. Alisema wawekezaji hukatishwa tamaa na milolongo ya kupata vibali husika, hivyo huamua kukimbilia nchi jirani ambazo sasa zinapiga hatua nzuri katika utalii. “Wenzetu wa Rwanda mwekezaji anapotaka kuwekeza katika sekta hiyo hupewa vibali kwa siku zisizopungua saba, sisi hapa kwetu huchukua zaidi ya mwaka mmoja, urasimu huu ndiyo unaotumaliza,” anasema. Kuhusu usalama wa watalii wawapo hifadhini, Dk Dembe anasema kikosi cha Polisi wa watalii kimeanzishwa na kwa kushirikiana na polisi jamii kitahakikisha watalii wanakuwa salama katika kipindi chote wanachotembelea hifadhi. Kwa mujibu wa tafsiri ya Kimataifa na ile ya Shirika la Utalii Duniani, mtalii ni mtu yoyote yule aneyesafiri kutoka katika maskani yake ya kawaida na kwenda sehemu nyingine na kukaa huko kwa zaidi ya saa 24 kwa madhumuni tofauti.

No comments: